Ujitokezaji wa Hejemonia Katika Asasi Za Kijamii: Mfano wa Dharau ya Ini, Msimu wa Vipepeo, Msururu wa Usaliti na Majilio ya Mkombozi

  • Harrison Onyango Ogutu; Dr. Sheila Wandera; Prof. Wendo Nabea Idara ya Lugha, Fasihi na Isimu, Chuo Kikuu cha Laikipia, Kenya
Keywords: Hejemoni, Hejemonia, Safu ya hejemonia, asasi za kijamii.

Abstract

Watu wenye uwezo na mamlaka wanatumia madaraka yao kuwatawala wengine kwa vishawishi anuwai. Asasi za kijamii kama vile ndoa, shule, vyuo, utamaduni na malezi zinaendelea kushuhudia utawala wa wenye uwezo juu ya wasio na uwezo. Licha ya ubayana wa hali hii katika jamii, watafiti na wahakiki wa tanzu za fasihi andishi hususan riwaya hawajaonyesha namna hejemonia inajitokeza katika asasi za kijamii. Ingawa wahakiki wengi wa riwaya wameweza kuangazia masuala ya kila nui kuhusu asasi za kijamii, suala la hejemonia katika taasisi hizo lilihitaji kumulikwa. Hivyo, utafiti huu ulidhamiria kuchunguza ujitokezaji wa hejemonia katika safu ya hejemonia ya jamii kwa mujibu wa riwaya za Msimu wa Vipepeo, Dharau ya Ini, Msururu wa Usaliti na Majilio ya Mkombozi. Utafiti huu uliongozwa na nadharia ya hejemonia ilioasisiwa na Antonio Gramsci katika makala aliyoyaandika akiwa gerezani kati ya mwaka wa 1923 na 1936. Nadharia hii inaelezea udumishaji wa uwezo na mamlaka ya tabaka moja kuu juu ya tabaka dogo kwa kutumia mikakati anuwai. Utafiti huu ulifanyiwa maktabani ambako utaratibu wa upekuzi wa yaliyomo ulitumika kukusanya data huku mbinu ya kithamano ikitumika kuchanganua data hiyo. Matokeo ya utafiti huu yatawafaa wahakiki na watafiti wa lugha na fasihi huku yakiweka wazi uwepo wa hejemonia katika asasi za jamii.

Published
2020-06-30
Section
Articles