Mbinu za Lugha Zinazotumiwa katika Matangazo ya Biashara ya Kampuni ya Safaricom.

  • Jane Kanini Maithya; Prof. Nabea Wendo; Prof. James Ogola Onyango
Keywords: matangazo ya biashara, safaricom, bidhaa

Abstract

Matangazo ya biashara hunuiwa kuwajuvya wateja kuhusu kuwepo kwa bidhaa za kampuni mbalimbali na kuwahimiza wanunue bidhaa hizo. Vahid na Esmae’li (2012) wanasema kuwa licha ya kutimiza lengo hilo, matangazo hayo vilevile hunuiwa kuchekesha, kupotosha au kuwadanganya wateja ili wavutiwe na bidhaa inayotangazwa. Hayo hutekelezwa kupitia kwa lugha inayotumiwa. Waundaji huteua mbinu za lugha zilizo na uwezo wa kuwafanya wateja watamani kununua bidhaa hata ikiwa hawazihitaji. Utafiti huu unachunguza mbinu za lugha zinazotumiwa katika matangazo ya biashara ya Kampuni ya Safaricom. Ni kampuni maarufu ya mawasiliano nchini Kenya inayotoa huduma mbalimbali za mawasiliano kama vile uuzaji wa aina mbalimbali za rununu, huduma za intaneti, M-pesa, M-shwari na kadhalika. Kampuni hiyo hutumia mbinu mbalimbali za lugha zinazoundwa kwa ubunifu mwingi kwa nia ya kuvuta nadhari ya wateja wake. Ingawa kuna tafiti mbalimbali zimefanywa kuhusu Kampuni ya Safaricom, hakuna utafiti umechunguza na kuzieleza mbinu hizo kwa kina, pengo ambalo limezibwa na utafiti huu. Data katika makala haya ilipatikana kutoka kwa mtandao wa intaneti ambapo mtafiti alipakua matangazo ya Safaricom aina ya picha na video. Alizitumia kutoa mifano ya mbinu mbalimbali zinazotumiwa kwenye kwenye matangazo hayo. Utafiti ulibainisha kuwa waundaji wa matangazo ya Safaricom hutumia mbinu mbalimbali za lugha zinazoundwa kwa ubunifu wa hali ya juu kwa nia ya kuwajuvya wateja kuhusu kuwepo kwa bidhaa na huduma zao na vilevile kuwavutia wazinunue.

Published
2020-09-30
Section
Articles