Dhima Katika Mawasiliano ya Ushairi wa Jando Katika Jamii ya Watachoni, Kaunti ya Bungoma

  • Richard Makhakha Iyaya; Prof. Nabea Wendo; Dkt. Gwachi J. Mayaka
Keywords: Maneno muhimu: Dhima, umuundo, ubabe-dume, jando, watahiriwa, majukumu, mawasiliano.

Abstract

Makala haya yalilenga kuchunguza dhima ya mawasiliano ya ushairi wa jando kwenye jamii ya Watachoni wa kaunti ya Bungoma. Utafiti uliendelezwa kwa muundo wa kimaelezo ya kiethnografia ulioangazia kanuni za mila, utamaduni na mahusiano ya kimawasiliano na athari zake kwa mitindo na lugha ya uwasilishaji ili kubainisha dhima yake.  Nadharia ya Baada ya Umuundo ya Derrida (1966) ilitumika kuchanganua miundo na kuonyesha kuwa matini hubainisha ukinzani wa ujumbe anaouhusisha mwasilishaji katika kazi yake. Nadharia ya ubabe-dume ya Maclennes (1998) pia ilitumika kuchunguza namna mitindo ya uwasilishaji na lugha katika mawasiliano ya ushairi wa jando unavyoathiri asasi za kijamii. Utafiti huu ulihusisha ukusanyaji wa deta moja kwa moja kutoka jamii ya Watachoni wakati wa shughuli za jando kwenye Kaunti ya Bungoma. Kundi lengwa lilikuwa watahiriwa, wazazi, wanaume na wanawake Watachoni na viongozi wa shughuli za jando. Tulitumia sampuli kusudio na sampuli nasibu tabakishi kubainisha ushairi na wasailiwa waliorejelewa kuyaainisha mawasiliano haya ya ushairi wa jando. Ushairi 16 na watafitiwa 45 walirejelewa kuyachanganua mawasiliano haya katika awamu zote za shughuli za jando. Deta iliyokusanywa ilirekodiwa, ikaandikwa na kutafsiriwa kutoka lugha ya Kitachoni hadi ya Kiswahili kisha ikachanganuliwa. Utafiti huu ulitumia mbinu za uchunguzaji nyanjani, mahojiano, mashauriano na wasimamizi na kuainisha habari zilizotokana na vyombo vya habari. Vifaa kama vile kamera za picha tuli na za kunasa sauti na video vilitumika kukusanyia deta na hatimaye kuziwasilisha kwa njia za maelezo na majedwali. Deta iliwasilishwa kwa njia ya maelezo na kufafanuliwa kwa kuzingatia malengo, nadharia na mipaka ya utafiti.

Published
2020-08-31
Section
Articles