Mtagusano Jamii kama Mkakati katika Utekelezaji wa Mtaala wa Umilisi katika Somo la Kiswahili Nchini Kenya
DOI:
https://doi.org/10.51317/6tmcp182Keywords:
Kiswahili, Ki-Vygotsky, Mtaala wa Umilisi, mkakati wa mtagusano jamii, scaffolding, ufunzaji na ujifunzaji, ZPDAbstract
Makala hii ilichunguza matumizi ya mkakati wa Mtagusano Jamii katika utekelezaji wa Elimu ya Umilisi katika somo la Kiswahili nchini Kenya. Kazi hii ilijiegemeza katika kuchunguza mkakati huu na namna unavyotumiwa na walimu kurahisisha ujifunzaji wa stadi nne za lugha; Kusoma, Kuandika, Kusikiliza na Kuzungumza na kusoma kwa ufasaha, hasa katika Gredi ya 1 hadi ya 4 katika shule za msingi eneo la Kaunti ndogo ya Kimilili, Kaunti ya Bungoma. Eneo hili liliteuliwa ili kuwakilisha maeneo mengine nchini. Vilevile, eneo hili limekuwa mojawapo ya Kaunti Ndogo ambazo zimekuwa zikirekodi matokeo yasiyoridhisha katika tathmini za mwigo wa Gredi ya 4. Washiriki waliteuliwa kwa kutumia sampuli nasibu na ya matabaka. Shule 30 ziliteuliwa kati ya shule 101 kimakusudi katika utafiti huu. Hususan, utafiti huu ulilenga kuchunguza namna mitagusano ya kijamii inavyowezeshwa na mwalimu darasani katika ujenzi wa uelewa katika Mtaala wa Umilisi katika somo la Kiswahili. Kazi hii ya utafiti iliongozwa na Nadharia ya Mtagusano Jamii iliyotokana na mawazo ya Vygotsky na ilitumia mkabala mseto. Data zilikusanywa kutoka kwa walimu waliojaza hojaji kisha mtafiti akatumia mwongozo wa utazamaji shirikishi, akishiriki vipindi na wanafunzi. Uchanganuzi wa data ulifanywa kimaelezo na kitakwimu. Majibu ya utafiti huu yanaashiria kuwa, kupitia kwa juhudi za walimu, wanafunzi wana uwezo wa kujenga maarifa kuhusu dhana kupitia kwa Mtagusano/ Ushirikiano Jamii wanapojifunza somo la Kiswahili kwenye Mtaala wa Umilisi. Kupitia kwa utafiti huu, ilibainika wazi kwamba utekelezwaji wa Mtaala wa Umilisi katika somo la Kiswahili unahitaji mkakati unaojenga ushirikiano baina ya mwanafunzi na wenzake, walimu na yaliyomo katika mchakato wa ujifunzaji, nao ni mkakati wa Ushirikiano Jamii.
Downloads
Published
Issue
Section
License
Copyright (c) 2026 Barasa Allan Wafula

This work is licensed under a Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 4.0 International License.