Ulinganishi wa Matatizo Ya Kijamii Yanayowakumba Majagina Katika Tendi Za Mikidadi Na Mayasa Na Kalevala

  • Jackson Ndung’u Mwangi
  • Prof. Wendo Nabea
  • Dr Sheila Wandera-Simwa
Keywords: Majagina, utendi, matatizo ya kijamii, motifu

Abstract

Uwepo wa tendi katika maeneo ya Afrika umezua mjadala na mgogoro mkali mno katika jamii ya usomi.  Hii ni kutokana na rai kuwa wasomi na watafiti wengi kutoka maeneo ya Kimagharibi walidai kuwa Afrika hakuna tendi ila kinachodaiwa kuitwa tendi ni masimulizi ya kisifo tu. Wahakiki wengine wamezifutilia mbali tendi hizi kwa kudai kuwa maudhui yake ni ya kichawi na sihiri. Pia, vigezo vya kuainisha tendi vilivyotumiwa na wanazuo wa Kimagharibi vilikuwa vya kimaeneo na kimakusudi, walidhalilisha tendi za Kiafrika. Licha ya kuwa kuliibuka watafiti wa Kiafrika na kudai kuwa Afrika kuna tendi, wao pia walielekea kutumia vigezo ambavyo ni vya kimaeneo. Ili kujaribu kutatua mzozo na utata uliopo kuhusu uwepo wa tendi katika maeneo ya Kiafrika, utafiti huu ulinuia kuchunguza iwapo kuna uwiano wa matatizo ya kijamii yanayowakumba majagina baina ya tendi za maeneo haya mawili. Madhumuni makuu yalikuwa kutathmini iwapo kuna uwiano wa matatizo ya kijamii yanayowakumba majagina baina ya tendi za Kiafrika na zile za Kimagharibi licha ya tendi za Kiafrika kufutiliwa mbali na baadhi ya wasomi wa Kimagharibi. Mtafiti alinua kutafiti tendi mbili ambazo ni Utendi wa Mikidadi na Mayasa unaopatikana Afrika na Utendi wa Kalevala unaopatikana Finland katika maeneo ya Kimagharibi. Utafiti huu uliongozwa na Nadharia ya Ruwaza ya Shujaa iliyoasisiwa Joseph Campbell (1987). Utafiti huu ni wa muundo wa kiudhamano na mahali pa utafiti palikuwa ni katika Maktaba. Inatarajiwa kuwa utafiti huu utakuwa mchango mkubwa kwa jamii ya wasomi hasa wanaoshughulikia fasihi linganishi na utajaribu kutatua ubishi ulioko kuhusu tendi za maeneo mbalimbali.

Published
2019-04-30
Section
Articles