Athari za Tafsiri ya Jazanda na Majazi kwa Mawasiliano: Mfano wa Tafsiri ya Riwaya ya Shetani Msalabani.

  • Magugu V. Njeru; Robert W. Oduori; Mark M. Kandagor Idara ya Kiswahili na Lugha nyingine za Kiafrika, Chuo Kikuu cha Moi
Keywords: Tafsiri, jazanda, majazi.

Abstract

Makala hii imeangazia jinsi vipengele vya jazanda na majazi vimetumika katika riwaya ya Ngũgĩ wa Thiong’o ya Caitaani Mutharaba-ini iliyoandikwa awali katika lugha ya Kikuyu na baadaye kutafsiriwa kwa Kiswahili na Kiingereza na mwandishi mwenyewe. Caitaani Mutharaba-ini, Shetani Msalabani na Devil on The Cross ziliteuliwa kimakusudi kwa kuzingatia umuhimu wake kama riwaya ya kwanza kuandikwa kwa Kikuyu na kutafsiriwa kwa Kiswahili na kiingereza, pamoja na ukwasi wake wa vipengele vya kijazanda na kimajazi. Sampuli ya data iliyochanganuliwa iliteuliwa kimakusudi kwa kujikita kwa mifano ya jazanda na majazi katika riwaya chanzi. Data iliyotumiwa katika kuandaa makala hii ilikusanywa kutokana na usomaji na uchanganuzi wa riwaya chanzi ya Kikuyu, tafsiri ya Kiswahili na ile ya Kiingereza. Data hii ilijikita kwa vipengele hivi vya jazanda na majazi. Uchanganuzi umejikita kwa jinsi mtafsiri alivyoshughulikia vipengele hivi kwa kuangazia jinsi vilivyotumika katika matini chanzi na namna vilivyohawilishwa katika tafsiri ya Kiswahili na ile ya Kiingereza. Katika kufanya hivi, utafiti umejiegemeza kwa nadharia ya baada ukoloni katika tafsiri hasa kipengele cha upekee wa lugha ya fasihi ya Kiafrika, iliyoandikwa na iliyotafsiriwa na kipengele cha uhusiano baina ya Lugha ya mtawaliwa na lugha ya mkoloni. Makala hii imebainisha kwamba licha ya kuwa nomino za pekee aghalabu hazitafsiriwi, katika miktadha ambamo zinabeba maana fiche kama ilivyo kwa majina ya kimajazi yaliyoangaziwa, huenda pana haja ya kutoa maelezo ili kufanikisha mawasiliano kamilifu.

Published
2022-02-28
Section
Articles