Mikakati ya Upole Katika Mawasiliano ya Wahudumu wa Magari ya Uchukuzi na Abiria katika lugha ya Kikamba.

  • Nicholas Kioko; Rose Mavisi; Dr. Justus Muusya (1.2.3) Catholic University of Eastern Africa, Kenya
Keywords: Mikakati ya upole, Wahudumu wa magari na abiria.

Abstract

Upole ni hali ya msemaji kudhihirisha kuwa anajali hisia na mahitaji ya msikilizaji katika mazungumzo. Mikakati ya upole hutumiwa na washiriki wa mazungumzo kulainisha na kufanikisha mazungumzo yao. Makala hii inachanganua mikakati ya upole inayotumiwa na wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma wanapoingiliana na abiria katika mji wa Matuu kwa kuzingatia lugha ya Kikamba. Mji wa Matuu upo katika kaunti ya Machakos, kaunti ndogo ya Yatta. Sampuli ya utafiti huu ilichaguliwa kimakusudi. Data ya utafiti huu ilikusanywa katika vituo vitatu vya magari ya uchukuzi katika mji wa Matuu vilivyoteuliwa kimakusudi. Mtafiti aliwahoji wahudumu ishirini na wawili na abiria kumi na tano. Mazungumzo kati ya wahudumu wa magari na abiria yalirekodiwa kwa kutumia kinasa sauti. Njia ya uchunguzi ilitumika kuchunguza mbinu ishara za kuwasiliana kama vile ishara za uso. Kauli zilizo na mikakati ya upole zilinakiliwa na kuwekwa kwenye makundi matano ya mikakati ya upole ili kuchanganuliwa. Makundi hayo ni: Mkakati wa kuwa kwenye rekodi, mkakati chanya wa upole, mkakati hasi wa upole, mkakati wa kuwa nje ya rekodi na mkakati wa kutosema chochote. Utafiti huu uliongozwa na mihimili ya Nadharia ya Upole ya Brown na Levinson (1978, 1987). Matokeo ya utafiti huu yameonyesha kuwa wahudumu walitumia mikakati yote tano ya upole ili kulainisha mawasiliano kati yao na abiria. Mkakati chanya wa upole na mkakati hasi wa upole ndiyo iliyotumika kwa wingi na katika vituo vyote vitatu. Kupitia utafiti huu mtafiti anaamini kuwa washikadau katika sekta ya uchukuzi watapata maarifa kuhusu mbinu za kuwasiliana na abiria ili kutimiza malengo yao. Vile vile, kazi hii itasaidia kuboresha matumizi ya lugha kati ya wanajamii pamoja na kuongezea maarifa yaliyomo kuhusiana na taaluma ya isimujamii.

Published
2021-10-30
Section
Articles