Usawiri wa Dini, Mila na Tamaduni za Kiafrika katika Riwaya za Babu Alipofufuka (2001) na Dunia Yao (2006) za Said Ahmed Mohamed na Bina-Adamu! (2002) ya Kyallo Wamitila.

  • Sylvester Kimugung; Dkt. Magdaline Wafula; Prof. Peter Simatei. Idara ya Lugha, Fasihi na Isimu, Chuo Kikuu cha Moi, Kenya.
Keywords: uhalisiamazingaombwe, kusawiri, urejelezi wa dini, mila na tamaduni.

Abstract

Utafiti huu unanuia kuchunguza masuala haya kwa kutumia nadharia ya uhalisiamazingaombwe. Nadharia ya Uhalisiamazingaombwe iliasisiwa na Franz Roh mwaka wa 1925 kama njia ya kukiuka uhalisia na kusawiri dunia ya kisasa iliyotata na ovyo, iliyobutuka, na iliyoparanganyika. Lengo la utafiti ni kuhakiki mitindo ya urejelezi wa dini, mila na tamaduni za Kiafrika na namna inavyowasilisha mivurugo ya jamii katika riwaya teule. Ili kutimiza malengo ya utafiti huu riwaya tatu zimeteuliwa kimaksudi: Babu Alipofufuka (2001) na Dunia Yao (2006) za Said Ahmed Mohamed, na Bina-Adamu! (2001) ya Kyallo Wamitila. Nadharia tete za utafiti ni kuwa riwaya teule zinasawiri mitindo ya uhalisiamazingaombwe ili kuakisi mivurugo ya jamii ya kisasa. Data za utafiti huu umetumia usampuli wa kimaksudi kwa kuzingatia mihimili ya nadharia ya Uhalisiamazingaombwe. Utafiti huu ni wa kimaktaba. Riwaya teule na tahakiki mbalimbali zilipatikana maktabani. Data zimechanganuliwa kwa kutumia mihimili ya nadharia ya uhalisiamazingaombwe na kisha kuwasilishwa kwa njia ya kinathari kwa kutumia madondoo mbalimbali. Utafiti huu ulibaini kuwa matumizi ya dini za Kiafrika zimeonyesha kuwa falsafa za kiafrika zilikuwa zinahakikisha uhusiano mwema baina ya viumbe wote ulimwenguni kuanzia Mungu, mizimu, mizuka, binadamu, vitu vilivyohai na visivyohai. Uhusiano huu ni tofauti na ule wa kimagharibi ambao umekuwa unasisitiza utengano na kusasabisha dunia ya kiulimwengu. Matumizi ya uduara wa wakati umehakikisha watu wameishi kwa usawa, heshima na umoja tofauti na mwelekeo wa kimagharibi wa kistari kimoja ambao ni kandamifu kupitia dhana za ubinafsi na ubepari. Kulikuweko na matumizi ya mila na tamaduni za kiafrika. Mila na tamaduni zilihakikisha kuna maisha mazuri kwa watu wote. Maajilio ya wakoloni yalisambaratisha maisha haya kwa athari hasi kwa malezi ya watoto, mavazi, vyakula na elimu. Utafiti huu ni muhimu kwa kuchangia taaluma kwa kuelewa matumizi ya mitindo ya uhalisiamazingaombwe na namna inavyowasilisha mivurugo ya jamii.

Published
2021-06-30
Section
Articles