Uchunguzi wa fani za lugha zilivyotumika kuibua changamoto za vijana katika riwaya teule za Kiswahili

  • Harrison Onyango Ogutu
Keywords: Changamoto za vijana, Fani za lugha, Uhalisia.

Abstract

Utafiti huu ulilenga kuchunguza namna mbinu mbalimbali za lugha zilivyotumika kuibua na kudhihirisha changamoto katika jamii. Utafiti huu ulielekezwa na nadharia ya uhalisia ambayo hushughulikia uwasilishi wa uhalisi na ukweli wa mambo katika fasihi. Imani ya mhalisia ni kwamba kazi ya fasihi huwaweka wanajamii katika ulimwengu wao wa kawaida, kweli na halisi. Mihimili ya uhalisia iliotumika katika utafiti huu ilikuwa; nguzo ya kielelezo inayosisitiza uigaji wa hali halisi kwa njia ya kweli, wazi na sahihi; nguzo ya matumizi ya lugha ya wakati uliopo na inayosheheni uhalisi na ukweli wa mambo kama yalivyo katika jamii husika ilitumika. Njia kuu ya utafiti huu ilikuwa utaratibu wa upekuzi wa yaliyomo katika ukusanyaji data. Mbinu ya kithamano ilitumika kuchanganua na kueleza data ya visa na matukio yaliyodhihirisha changamoto dhidi ya vijana. Utafiti huu   ulijikita   katika   muundo   wa   kimaelezi   ambao   ni   sahili   na   kueleza   mambo yanavyojitokeza kwa uyakinifu. Utafiti huu ulilenga wahusika vijana na changamoto zilizowakabili. Mtafiti alitumia sampuli ya kimaksudi ambapo riwaya alizozifanyia utafiti aliziteua kwa kudhamiria kuwa zilisheheni maudhui mengi yaliyohusu changamoto halisi zilizowakabili vijana katika jamii yao. Data iliyokusanywa ilijumuisha maudhui yenye changamoto halisi zilizowakabili vijana kama vile ufisadi, ubaguzi, umaskini na ukabila. Changamoto hizo zilisababisha athari kama vile kuacha masomo, mimba za mapema, majeraha na vifo. Utafiti huu ulinuia kuwa na natija kwa wasomi, wahakiki na watafiti wa masuala ya lugha na fasihi kwa kuwa sehemu ya kurejelewa. Aidha, matokeo ya utafiti huu yalitoa hamasisho kwa jamii kuhusu changamoto za vijana ili kusaidia kutafuta suluhu kwa changamoto hizo.

Published
2021-02-28
Section
Articles